JAFO EDUCATION FOUNDATION KUNUNUA KILA ‘A’ , DIVISION ONE KUTUNUKIWA DONGE NONO KISARAWE.
Kisarawe, Mei 23, 2026 Mwenyekiti wa Jafo Education Foundation na Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, ametangaza motisha mbalimbali kwa walimu na wanafunzi wa Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuongeza ari ya kufundisha na kujifunza, hatua inayotarajiwa kuimarisha kiwango cha ufaulu katika shule za wilaya hiyo. Dkt. Jafo ametoa ahadi hizo leo alipohudhuria Kongamano la Elimu la Kata ya Kisarawe, lililowakutanisha viongozi, walimu, wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu kujadili mikakati ya kuboresha ufaulu na maendeleo ya sekta ya elimu. Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Jafo aliwapongeza viongozi wa Kata ya Kisarawe kwa ubunifu na juhudi zao za kuandaa kongamano hilo, akieleza kuwa limeonyesha namna ambavyo jamii inaweza kushirikiana katika kuleta mabadiliko chanya kwenye elimu. "Nawapongeza viongozi wa Kata ya Kisarawe kwa kuandaa kongamano hili muhimu. Huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na kata zingine kwa sababu maendeleo ya elimu yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu," alisema Dkt. Jafo. Katika kuhamasisha ufaulu kwa wanafunzi, Dkt. Jafo ametangaza kuwa kupitia Jafo Education Foundation, kila mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka Shule za Sekondari Chanzige na Kimani atakayefaulu kwa Division One atapatiwa zawadi ya Shilingi 300,000 ili imuwezeshe kununua vifaa vya kujiunga na masomo ya kidato cha tano ikiwa ni motisha ya kufanya vizuri katika masomo Aidha, akionga na vijana wa kidato cha tano ambao mwakani watafanya mitihani yao ya kidato cha sita amesema "mwanafunzi yeyote wa kidato cha sita wa shule ya Minaki na Shule ya Kimani zilizopo katika Kata ya Kisarawe atakayepata Division one ya Point 3 kwa mitihani itakayofanyika mwezi Mei 2027 atapata ufadhili wa kulipiwa ada ya Chuo Kikuu kwa mwaka wa kwanza kupitia Jafo Education Foundation. Kwa upande wa walimu, Dkt. Jafo ametangaza mpango maalum wa motisha kwa walimu utakaotekelezwa na Jafo Education Foundation kwamba kwa mitihani ya Kidato cha nne, mwalimu aliyewezesha mwanafunzi kupata A katika somo lake atalipwa Shilingi 50,000 kwa kila A iliyopatikana. Mpango huo unalenga kuongeza hamasa kwa walimu kuendelea kufundisha kwa bidii, ubunifu na kujituma zaidi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa. Dkt. Jafo pia ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu kwa kutoa msaada wa hali na mali ili kuhakikisha Kisarawe inaendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu na kuwa miongoni mwa wilaya zinazofanya vizuri kitaaluma nchini. "Tuna wajibu wa kuwekeza katika elimu kwa sababu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yetu. Kupitia Jafo Education Foundation tutaendelea kuwaunga mkono walimu na wanafunzi ili kufikia malengo makubwa zaidi ya kielimu," alisisitiza. Tangazo la motisha hizo limepokelewa kwa furaha na shangwe na walimu, wanafunzi pamoja na wazazi waliohudhuria kongamano hilo, huku wengi wakieleza kuwa hatua hiyo itachochea ushindani wa kitaaluma na kuongeza ari ya kufikia matokeo bora zaidi katika shule za Kisarawe.
Read More